Kwaya ya Dar City imefanikiwa kuibuka kinara katika mashindano ya kwaya yaliyofanyika usiku wa kuamkia Agosti 26, 2025 katika Ukumbi wa Police Mess hapa Jijini Tanga ambapo mashindano ya SHIMISEMITA 2025 yanaendelea.
Jumla ya kwaya 21 zilishiriki katika mashindano hayo ambapo kwaya ya Dar City iliibuka kidedea kutokana na kuwa na kuonesha upekee wa sauti, mpangilio wa nyimbo na ubunifu wa hali ya juu huku wakiibua shangwe yenye hisia kali miongoni mwa mashabiki na watazamaji waliojitokeza.
Aidha, mbali na ubora wa uimbaji kwaya ya Dar City imeonesha umahiri wa uvaaji baada ya kuwa na muonekano mzuri kwani kwaya nzima ilikuwa imevaa sare ya suti ambayo ilichagiza muonekano mzuri wa utanashati pamoja na kuvutia hadhira.
Kwa matokeo hayo, Dar City inaendelea kubaki kileleni kama kwaya inayoongoza kwa ubora na inaendelea kuandika historia mpya ndani ya mashindano ya SHIMISEMITA, ikiendelea kuweka alama ya kumbukumbu kwa mashabiki wake na kwa tasnia ya kwaya nchini.
Mashindano ya SHIMISEMITA 2025 bado yanaendelea katika Jiji la Tanga ambapo Agosti 29,2025 inatarajiwa kuwa kilele cha mashindano haya huku tayari Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ikiwa na mwendelezo mzuri wa ushiriki hadi sasa ambapo imefanikiwa kufika kwenye hatua za mtoano kwa baadhi ya michezo.
Katika mashindano haya ya SHIMISEMITA 2025 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeendelea kuunga mkono kauli mbiu ya Mashindano ya mwaka huu ambayo inasema "Jitokeze Kupiga Kura kwa Maendeleo ya Michezo".
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.