Na: Doina Mwambagi
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Ndugu Elihuruma Mabelya, leo tarehe 15 Agosti 2025, ameongoza kikao cha ndani na watumishi wa Halmashauri kilichofanyika katika Ukumbi wa Karimjee, kwa lengo la kujadili utekelezaji wa majukumu, kuboresha maslahi ya watumishi, na kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
Akizungumza katika kikao hicho, Mabelya amewashukuru watumishi kwa mshikamano na juhudi walizoonesha katika mwaka wa fedha uliopita, hatua iliyochangia ongezeko la makusanyo ya mapato ya Halmashauri.
“Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri imelenga kufikia makusanyo ya shilingi bilioni 156. Niwaombe watumishi wenzangu twendeni tukafanye kazi kwa bidii, ubunifu na uzalendo, tukifuata kanuni na sheria ili tufanikishe malengo haya muhimu kwa maslahi mapana ya wananchi, kwani asilimia 70 ya mapato yanarudi kwenye miradi ya maendeleo na asilimia 30 ni kwa ajili ya matumizi mengine ya Halmashauri,” amesisitiza Mabelya.
Aidha, Mkurugenzi Mabelya ameeleza kuwa Halmashauri imeadhimia kuboresha maslahi ya watumishi wake ili kuongeza ufanisi katika kazi, kwa kuhakikisha mazingira bora ya kazi, upatikanaji wa vifaa muhimu, na kutoa mafunzo endelevu yatakayoongeza tija.
Sambamba na hilo Ndugu Mabelya amewahakikishia watumishi hao kufanya nao vikao kila baada ya robo ya mwaka kwa lengo la kujafdili maendeleo ya kazi, kushughulikia changamoto, na kuimarisha mshikamano wa pamoja katika utekelezaji wa majukumu.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Katibu Tawala wa Ilala, viongozi na watumishi kutoka idara mbalimbali katika Halmashauri hiyo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.