Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo, ametoa wito kwa wanawake wa Wilaya ya Ilala kuepuka mikopo kutoka taasisi za kifedha zenye masharti kandamizi, akibainisha kuwa mikopo hiyo imekuwa chanzo cha migogoro ya kifamilia na kuwakwamisha kiuchumi.
Wito huo umetolewa katika kongamano la uelimishaji kwa vikundi juu ya mikopo ya asilimia kumi kupitia mfumo jumuishi, lililowakutanisha wanawake kutoka kata 36 za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mpogolo amesema mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam haina riba na inalenga kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujikwamua kimaisha. “Mikopo hii itatolewa kwa uwazi na kwa kufuata utaratibu mpya ulioidhinishwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ambao unahakikisha waombaji wote wanazingatia sifa, uthibitisho na uwajibikaji. Hivyo wanawake, mlango uko wazi,” alisema.
Ameongeza kuwa zaidi ya vikundi 440 kati ya 945 vilivyoomba mikopo hiyo tayari vimekidhi vigezo na vinatarajiwa kupokea fedha ndani ya siku saba. Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhamasisha utoaji wa mikopo hiyo kwa uwazi na usawa kwa vikundi vyote vinavyostahili.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Bw. Charangwa Selemani, amesema baadhi ya vikundi vilichelewa kupokea mikopo kutokana na changamoto kama ukosefu wa uhalisia wa miradi, taarifa zisizo sahihi, na uzoefu mdogo wa biashara. Wanawake walioshiriki kongamano hilo walieleza shukrani zao kwa Rais Samia kwa kuendeleza mpango huo wa kuwawezesha wananchi kiuchumi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.