Na: Hashim Jumbe
Kamati ya Uchumi na Huduma za Jamii, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo tarehe 14 Februari, 2022 imefanya ziara ya ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo iliyotekelezwa kwa kipindi cha robo ya Pili iliyoanzia Oktoba na kuishia Disemba, 2021.
Ziara hiyo ya kawaida yenye lengo la kuwapa fursa wajumbe wa Kamati hiyo kuweza kukagua na kutolea mapendekezo Miradi ya Maendeleo iliyotekelezwa na Halmashauri kwa kipindi cha robo ya Pili katika Sekta za Elimu, Afya, Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na kufuatilia vikundi vilivyonufaika na 10% ya fedha za Mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Wakiwa kwenye ziara hiyo leo, Kamati ilikagua ujenzi wa mabucha ya nyama yanayojengwa Vingunguti, kama anavyoeleza Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Steven Mushi "leo kamati tulikuwa na ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo ambayo imefanyika katika Jiji la Dar es Salaam, tulianza na mradi wa mabucha ambao una thamani ya Shilingi Milioni 300, tumefika na tumekuta ipo katika hali nzuri teyari kwa ajili ya matumizi na muda siyo mrefu yataanza"
Aidha, Kamati hiyo ilipata pia nafasi ya kutembelea kikundi cha usindikaji wa ndizi kinachoitwa 'Banana Group' kilichopo Vingunguti, ambapo Kamati ilijionea namna ndizi zinavyovundikwa, zinavyopokelewa na kutayarishwa mpaka zinapoiva, kikundi hicho ni moja kati ya vikundi vilivyonufaika na 10% ya Mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Mwisho, kamati hiyo ilitembelea pia ujenzi wa Vyumba Nane (8) vya Madarasa Shule ya Sekondari Bangulo vilivyojengwa kwa fedha za UVIKO-19 pamoja na ujenzi wa matundu kumi (10) ya vyoo yanayojengwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri.
Ziara hiyo ilitamatishwa na majumuisho ambapo Mhe. Mushi alitoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita (6) ikiongozwa na Mhe. Rais Samia kwa kutoa fedha za miradi, Mstahiki Meya, Madiwani pamoja na timu ya wataalamu wa Jiji la Dar es Salaam "tunampongeza Mama yetu, Mhe. Samia kwa namna ambavyo anavyoachia fedha za miradi na tunaipongeza Halmashauri inavyojitahidi kwenye mapato yake ya ndani na kwenye ile 10% ya mikopo ya wanawake, vijana na walemavu"
Itakumbukwa kuwa ziara hiyo ni ya kisheria na itafuatiwa na kikao cha Kamati kwa ajili ya kujadili taarifa za utendaji kazi pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2021
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 2128800
Namba ya Mkononi: 0713614364
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.